IQNA

Maadili katika Qur'ani Tukufu /13

Kinachomfanya mwanadamu kusahau Akhera

18:56 - July 16, 2023
Habari ID: 3477290
TEHRAN (IQNA) – Kusahau ukweli kwamba akhera itakuwa makazi yetu ya milele kumekatazwa katika Qur'ani Tukufu na Hadithi kutoka kwa Mtume Muhammad (SAW) na Ahul Bayt (AS).

Kila tabia haibuki au kuundwa mara moja bali baada ya muda na kupitia utangulizi. Kuzidishiwa matamania na anasa ni miongoni mwa mambo ya kutangulia kusahau akhera.

Neno la Kiarabu la kutamani ni ‘Amany’ ambalo maana yake asilia ni tathmini. Mwanadamu katika fikra zake hutathmini baadhi ya masuala na ndiyo maana matamanio yaliyorefushwa na matamshi yasiyo na msingi hutajwa kuwa Amany.

Mwenyezi Mungu, katika Aya ya 14 ya Sura Al-Hadid, alieleza matamanio yaliyorefushwa kuwa mojawapo ya mambo yanayowadanganya wanadamu: “Watawaita wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu."

Kinachopaswa kuzingatiwa ni kwamba kuwa na matamanio yenyewe sio mbaya bali kuna tofauti kati ya matamanio ya kawaida na matamanio yaliyorefushwa.

Kinachotofautisha kati ya hayo mawili ni kukumbuka kifo na masuala ya kiroho.

Katika matamanio ya kawaida, mtu hufanya juhudi kufikia matamanio yake kwa kupanga vizuri na kutekeleza mipango lakini wakati huo huo hamsahau Mwenyezi Mungu na mambo ya kiroho. Anajua kwamba Mwenyezi Mungu huona chochote anachofanya na hivyo huepuka kutumia njia zisizo halali au kinyume na maadili ya kidini ili kufikia matamanio yake.

Lakini sivyo hivyo katika matamanio yaliyorefushwa ambapo mtu hufikiri kwamba ataishi maisha marefu na kuelekeza nguvu zake zote katika kufikia matamanio ya kidunia kwa njia yoyote inayowezekana. Hatumii wakati wowote kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kifo.

Imam Ali (AS) anawaambia watu wa aina hiyo kwamba wajiepushe na kudanganywa na matamanio kwani wapo watu wengi sana waliotamani siku wapate baraka tele na hawakuifikia, na walikuwa wengi sana ambao walijenga majumba lakini hawakupata fursa ya kuishi kwenye majumba hayo na watu wengi sana ambao walikusanya mali nyingi lakini hawakufanikiwa kunufaika nazo.

Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) anaelezea kwa uzuri uhusiano kati ya matamanio ya kurefushwa na kifo. Mtume (SAW) alipokuwa akitoa nasaha kwa maswahaba zake, alichora mistari sambamba na kisha mstari wa wima, akiwauliza maana ya mistari hiyo. Maswahaba wakasema hawajui.

Mtukufu Mtume (SAW) alisema mistari sambamba ni kama matamanio ya mtu yaliyopanuliwa (ambayo hayana mwisho) na mstari wa wima unawakilisha kifo ambacho hukata tamaa zote hizo.

captcha