IQNA

Ifahamu Qur'ani Tukufu /3

Misingi mbali mbali ya Mwongozo katika Qur'ani Tukufu

21:27 - May 30, 2023
Habari ID: 3477070
TEHRAN (IQNA) - Wengine wanajaribu kuweka mipaka ya mwongozo wa Qur'an Tukufu kwenye uwanja fulani katika hali ambayo kuna vipengele mbalimbali vya mwongozo vinavyoonekana katika kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu.

Muongozo wa Qur'ani Tukufu haukomei kwenye uwanja fulani wa maisha ya mwanadamu bali unahusu nyanja zote za maisha. Kwa maneno mengine, sio kwamba Qur'ani Tukufu inamuongoza mwanadamu katika eneo moja la maisha yake na haimpi bila majibu wala mwongozo katika maeneo mengine.

Qur'an Tukufu ina mamlaka katika nyanja zote za maisha na mahitaji ya mwanadamu, kuanzia ukuaji wa kiroho na ukamilifu wa mtu, ambao ni hitaji la juu kabisa, hadi suala la kuendesha jamii za wanadamu, kushikilia uadilifu, usimamizi, kuwafukuza maadui mbalimbali, kulea watoto, nk.

Qur’an inaposema: “Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu." (Aya ya 34 ya Surah Fussilat)

Qur'ani Tukufu inasema hivi kuhusu familia: “Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.” ( Aya ya 74 ya Surah Al-Furqan)  Na pia: “Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.." (Aya ya 32 ya Surah An-Nur)

Na kuhusu amani ya kiroho ambayo ni miongoni mwa mahitaji makuu ya kila mwanadamu, Qur'ani Tukufu inasema: “Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na Waumini. (Aya ya 26 ya Suratul-Fath)

Qur'ani Tukufu inahimiza kutafuta elimu na kujua maumbile. Pia ina mapendekezo kuhusu tabia za kibinafsi za mtu: "Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda." (Aya ya 18-19 ya Surah Luqman)

Kwa hiyo kuhusu masuala kama haya, ambayo yanajumuisha nyanja zote za maisha, Qur'ani Tukufu inatoa mafunzo na mwongozo. Ndiyo kusema, Qur'ani Tukufu inashughulikia nyanja zote za maisha ya mwanadamu na ina muongozo na mafunzo kwa nyanja zote za maisha yake.

Ni wazembe kiasi gani baadhi ya watu wanaodhani kuwa Qur'ani Tukufu haina la kusema kuhusu masuala ya maisha, siasa, uchumi, utawala n.k. Hapana si hivyo kwa sababu sehemu kubwa ya Qur'ani Tukufu inahusu masuala ya maisha ya kila siku.

captcha