IQNA

Kitabu cha maisha ya Shahidi Soleimani chazinduliwa, dibaji imeandikwa na Kiongozi Muadhamu

23:47 - January 03, 2021
Habari ID: 3473519
TEHRAN (IQNA) - kitabu cha maisha ya Shahidi Qassem Soleimani, alichoandika yeye mwenyewe kiitwacho "Nilikuwa Sihofu Chochote" kimezinduliwa leo.

Kitabu hicho kimepambwa kwa dibaji iliyoalifiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Katika sehemu ya dibaji hiyo, Kiongozi Muadhamu ameandika: “Kila ambacho kinahuisha kumbukumbu ya shahidi wetu azizi kinavutia macho na moyo.”

Kitabu hicho kina kurasa 136 na ni kitabu cha kwanza kuchapishwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Haj Qassem ambayo ina jukumu la kuchapisha vitabu, makala, n.k kumhusu shahidi hiyo.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alielekea Iraq Januari 3 mwaka 2020 kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano na maadui pamoja na magaidi na pia katika kuangamiza kundi la kigaidi la Daesh au ISIS. Pia alikuwa nguzo muhimu katika harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. Halikadhalika alikuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha njama ya Marekani na Wazayuni ya kuligawa eneo vipande vipande.

3473587

captcha