IQNA

Rangi ya njano yatumiwa kueneza umoja wa Wakristo, Waislamu Kenya

10:21 - August 17, 2016
Habari ID: 3470528
Maeneo kadhaa ya Ibada katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi yamepakwa rangi ya njano kama njia ya kuleta umoja na kusisitiza nukta za pamoja baina ya wafuasi wa dini mbali mbali.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, maeneo ya ibada yaliyopkwa rangi ya njano ni pamoja na Misikiti, Makanisa na Mahekalu ya Wahindu mjini Nairobi. Rangi ya njano ambayo ni nembo ya mapenzi imepakwa katika maeneo hayo ya ibada.

Fikra ya ‘rangi katika ibada’ ilianzishwa na Yazmany Arboleda, Mmarekani mwenye asili ya Colombia ambaye anasema: "Lengo ni kutumia maeneo ya ibada Kenya kueneza ujumbe wa upendo kwa kupaka rangi ya njano.” Anasema fikra yake kutoka mwanzo ni "kubadilisha majengo ya ibada kuwa sehemu za kuzungumza kuhusu ubinadamu wetu wa pamoja.”

Anasema awali haikuwa rahisi kuwakinaisha Maimamu na Mapasta kuunga mkono mradi huo lakini baadaye wengi waliafiki maeneo yao ya ibada kupakwa rangi ya njano. Anasema msimamizi mmoja wa msikiti alitaka ushahidi kuwa njano ni rangi ya Kiislamu huku kanisa moja akitaka msaada wa kifedha kabla ya kushiriki katika mradi huo.

Anasema taasisi ya kwanza ya kidini kuunga mkono mradio huo ni kamati ya Msikiti wa Jeddah Kambi katika eneo la Kibra mjini Nairobi. Msikiti huo ulipakwa rangi ya njano Septemba mwaka 2015.

Arboleda amebainisha matumaini yake kuwa mradi wake utapelekea kuwepo maelewano na wafausia wa dini zote Kenya na dunia nzima kuishi kwa amani.

3523357

captcha