IQNA

Mazungumzo baina ya dini

Msikiti wa Jamia Nairobi wakaribisha wasiokuwa Waislamu kuwaelimisha

19:01 - June 06, 2023
Habari ID: 3477106
Msikiti wa Jamia katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi hivi karibuni umeandaa siku maalumu ya kuwakaribisha wasiokuwa Waislamu, hasa Wakristo nchini humo, ndani ya msikiti huo ili waweze kujifunza kuhusu Uislamu na Waislamu na kuondoa fikra potovu zilizopo.

Wakati wa program hiyo ya Jumamosi iliyopewa jina la "Siku ya Wazi', uongozi wa msikiti huo umewakaribisha Wakenya wa dini zote kutembelea msikiti, kufahamu mengi kuhusu Uislamu kwa kuuliza maswali kisha kupata majibu kutoka kwa wasomi wa dini hiyo.

Kwa mujibu wa Imam wa Jamia Sheikh Jamaldin Osman wamefungua milango ya msikiti ili kuleta uelewano na kuwezesha wengi kufahamu dini hiyo.

Sheikh Osman ametaja ubaguzi, fitina na ukabila akisema ni kati ya mambo ambayo yatatokomezwa iwapo kila dini itafungua milango kwa wale ambao si waumini wake kufahamu yaliyomo.

“Sisi hatulazimishi mtu kuingia Kusilimu lakini binadamu ana hiari kuingia Uislamu. Mimi nina jukumu la kufundisha ukweli kuhusu dini hii badala ya dhana zinazoenzwa si kweli. Wakristo na Waislamu wote wapo katika nchi kwa hivyo heshima na maelewano inapatikana tukitangamana na kufahamiana,” akasema Sheikh Osman.

Akizungumza na gazeti la kila siku la Taifa Leo la nchini Kenya, Mkuu wa Daawa (Ulinganiaji) Mohamed Sheikh alisema zaidi ya Wakenya 700 walijitokeza katika msikiti huo ili kupata mafunzo na kujua mengi kuhusu Uislamu.

Waislamu ni jamii ya walio wachache nchini Kenya ambapo wanakadiriwa kuwa asilimia 25-30 ya watu wote nchini humo. Waislamu  wana nafasi kubwa na yenye ushawishi nchini humo Kenya na kwa kiasi fulani kutokana na idadi yao kubwa, hali hii pia inahusiana na ukweli kwamba Waislamu kwa ujumla wanaishi katika maeneo muhimu ya kiuchumi na kimkakati ya pwani na kaskazini mashariki. Pamoja na hayo kutokana na sera za kikoloni na wamishonari wakristo kutoka nchi za kikoloni barani Ulaya na Amerika kumekuwa na propaganda potovu dhidi ya Waislamu wa Kenya kwa lengo la kuibua mifarakano nchini humo. Ili kukabiliana na wimbi hilo la upotoshaji,  Waislamu wote nchini Kenya, wakiwemo wa madhehebu za Shia na Sunni wamekuwa mstari wa mbele kuwaslisha taswira sahihi ya Uislamu nchini humo.

4145972

 

captcha