IQNA

Hija

Mkutano wa maandalizi ya Hija wafanyika Madina

9:48 - May 11, 2023
Habari ID: 3476988
TEHRAN (IQNA) – Kikao kimefanyika katika mji mtakatifu wa Madina nchini Saudi Arabia ambapo maafisa wametathmini maandalizi ya msimu ujao wa Hija.

Gavana wa Madina, Mwanamfalme Faisal bin Salman, ambaye pia anaongoza kamati ya Hija na ziara katika kanda hiyo, wiki hii aliongoza kikao cha jopo hilo na kujadili mipango ya operesheni itakayofanywa na mashirika ya serikali wakati wa msimu wa hija.

Msimu wa Hajj unatarajiwa kuanza Juni 26.

Alisisitiza umuhimu wa utayarifu kamili kwa msimu wa kila mwaka kwani idadi ya mahujaji wa Hajj mwaka huu inatazamiwa kurudi kwa wale kabla ya janga la ulimwengu.

Mkutano huo ulipitia, pamoja na mambo mengine, mpango wa operesheni kwa tawi la Wizara ya Hijja huko Madina ambao unajumuisha maandalizi ya kupokea karibu mahujaji milioni 1.8 wa ng'ambo wakati wa msimu wa Hijja.

Uwezo wa malazi wa hoteli za Madina karibu na Msikiti wa Mtume SAW, mahali pa pili patakatifu pa Uislamu, ulichunguzwa pia.

Jambo lingine katika ajenda ilikuwa mpango wa operesheni ya Hija kwa uwanja wa ndege wa Mwanamfalme Mohammed bin Abdulaziz huko Madina ambapo trafiki wakati wa Hija inatarajiwa kuongezeka kwa karibu asilimia 136 ikilinganishwa na mwaka jana.

Al Rawda Al Sharifa

Baada ya kutekeleza ibada ya Hijja, mahujaji kwa kawaida hukusanyika Madina kuswali katika Msikiti wa Mtume SAW ambao ni maarufu kama Al-Masjid an-Nabawi , ilipo Al Rawda Al Sharifa ambapo kaburi la Mtume Muhammad (SAW) liko.

Wizara ya Hija ya Saudia imesema kwamba kipaumbele cha kujiandikisha kuhiji mwaka huu kinatolewa kwa Waislamu ambao hawakufanya ibada hiyo hapo awali.

Ufalme umesema hakutakuwa na kikomo kwa idadi ya mahujaji kutoka kote ulimwenguni kwa msimu ujao wa Hija.

Katika miaka miwili iliyopita, Saudi Arabia ilipunguza idadi ya Waislamu wanaoruhusiwa kutekeleza ibada ya Hija ili kuzuia kuenea kwa COVID-19.

Takriban Waislamu milioni 2.5 walikuwa wakihudhuria Hijja kila mwaka katika nyakati za kabla ya janga hilo.

Waislamu, ambao wana uwezo wa kimwili na kifedha, wanapaswa kuitekeleza angalau mara moja katika maisha.

3483503

Kishikizo: hija saudi arabia
captcha