IQNA

Jinai za Israel

UN: Makazi Haramu ya Waisraeli ni Kikwazo Kikubwa cha Amani

19:27 - August 26, 2022
Habari ID: 3475685
TEHRAN (IQNA) - Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amesisitiza uharamu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni wa Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina na kubainisha kuwa hatua hiyo ni kikwazo kikubwa cha amani.

Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati, Tor Wennesland, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

"Vurugu za kila siku pia zimeendelea katika viwango vya juu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa," alisema.

Akibaini kuwa ni machache sana yanayofanywa kuhusiana na uchunguzi na mashtaka ya ghasia na jinai zinazotekelezwa walowezi, Wennesland alitoa wito wa kuwawajibisha wahalifu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha amevitaka vikosi vya Israel  viache kutumia "nguvu za kikatili" dhidi ya Wapalestina.

Halikadhalika amesema vurugu zimeongezeka katika sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel. Israel inaendelea kujenga vitongoji vya walowezi pamoja na kubomoa nyumba za Wapalestina na kuwafukuza kutoka ardhi zao za jadi.

Wennesland alidokeza kwamba utawala ghasibu na vamizi wa Israel ulibomoa majengo au kuwalazimisha wamiliki kubomoa majengo 78 yanayomilikiwa na Wapalestina katika eneo la C na 18 huko Quds (Jerusalem) Mashariki, na kuwafanya Wapalestina 103 wakiwemo watoto 50 kuyahama makazi yao. Pia walibomoa nyumba mbili zilizokuwa na familia nyingi katika kijiji cha Qarawat Bani Hassan, karibu na Salfit katika eneo B, na kusababisha uharibifu kwa nyumba tatu za jirani na kuwafukuza watu 18, wakiwemo watoto kumi.

Aliongeza kuwa utawala ghasibu wa Israel pia ulibomoa nyumba mbili katika kijiji cha Rummana, karibu na Jenin katika eneo B na kusababisha watu 13 wakiwemo watoto wanne kuyahama makazi yao.

Ametoa wito kwa mamlaka za Israel kukomesha ubomoaji wa mali zinazomilikiwa na Wapalestina na kuhamishwa na kufukuzwa kwa Wapalestina.

Israel ilikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, likiwemo eneo la magharibi mwa mji mtakatifu wa al-Quds, mwaka 1967. Baadaye iliiteka Quds Mashariki, ambayo Wapalestina wanataka kuwa mji mkuu wa taifa lao la baadaye.

Kati ya Waisraeli 600,000 na 750,000 wanamiliki zaidi ya makazi 250 haramu ambayo yamejengwa katika Ukingo wa Magharibi tangu uvamizi wa 1967.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika maazimio kadhaa limelaani miradi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa kifalme ya Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina huku ukipuuza takwa la jamii ya kimataifa la kusimamisha ujenzi huo kwa kukingiwa kifua na Marekani. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.  

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hadi sasa utawala wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

3480220

 

captcha