IQNA

Palestina yalalamika katika Umoja wa Mataifa kuhusu jinai za Israel

21:39 - December 30, 2020
Habari ID: 3473508
TEHRAN (IQNA)- Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ametuma barua tofauti kwa viongozi wa umoja huo akitaka jamii ya kimataifa kukabiliana ipasavyo na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuuadhibu utawala huo kwa hatua yake ya kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.

Riyadh Mansour amewatumia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo akisisitiza kuwa: ujenzi wa vitongoji unaofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Quds ni kinyume cha sheria na unakiuka sheria za kimataifa. 

Mwakilishi wa Palestina katika Baraza la Usalama  ameitolea wito jamii ya kimataifa kuingilia kati suala hilo ili Mwaka Mpya wa 2021 Miladia ufanywe kuwa mwaka wa kusitishwa sheria inayoulinda na kuupatia kinga ya kutoshtakiwa utawala wa Kizayuni. 

Riyadh Mansour ametahadharisha kuwa, masuala ya kukosekana uadilifu na kuupatia kinga ya kutoshtakiwa utawala huo yataendelea iwapo utawala wa Kizayuni hautaadhibiwa; jambo ambalo litawazidishia masaibu tu na mateso wananchi wa Palestina, na kufuta matumaini ya kupatikana njia ya ufumbuzi wa kiadilifu wa mzozo kati ya Palestina na Israel. 

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa aidha ameashiria mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika hospitali na maeneo ya raia huko Ghaza na kueleza kuwa: mashambulizi ya utawala huo yameyatia hatarini maisha ya wagonjwa, watoto na raia wa Kipalestina. 

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la UN, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala wa Kizayuni ni kinyume na sheria; hata hivyo utawala huo ghasibu unaendeleza vitendo vyake vya mabavu na kujitanua kwa kubomoa nyumba za Wapalestina na kupanua ujenzi wa vitongoji hivyo. Utawala wa Israel umepata kiburi na kukiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa na uungaji mkono unaopata kutoka utawala wa Marekani.

3944350

captcha