IQNA

Utawala wa Israel kujenga vitongoji vipya vya walowezi katika ardhi za Palestina

20:07 - January 11, 2021
Habari ID: 3473545
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni wa Israel umeongeza maradufu kasi ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ulizowapora Wapalestina hatua ambayo itaibua msuguano na serikali mpya ijayo ya Marekani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema katika taarifa yake kwamba hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuongeza kasi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina huko Baytul Muqaddas ni jinai ya kivita kama ambavyo pia ni jinai dhidi ya haki za binadamu za Wapalestina na ni kukanyaga waziwazi sheria za kimataifa.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umekusudia kufuta fursa zote za kuundwa nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Quds.

Taarifa hiyo imelalamikia pia kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya uvunjaji huo mkubwa wa sheria za kimtaifa unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema kuwa, katika kipindi cha wiki za hivi karibuni, na kwa kutumia fursa ya siku za mwishoni mwa utawala wa Donald Trump huko Marekani, Wazayuni wamezidisha jinai zao dhidi ya Wapalestina, kuvunja nyumba zao, kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuwateka nyara vijana wa taifa madhlumu la Palestina katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Utawala wa Kizayuni wa Israel una nia ya kujenga zaidi ya nyumba laki 4 nyingine katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwa ni muendelezo wa kupora ardhi za wananchi wanaodhulumiwa kila upande wa taifa la Palestina.

Utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao unapata himaya kamili ya Marekani, umekiuka azimio 2334 la Baraza la Usalama, ambalo Disemba 2016 lilitaka usitishwaji wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. 

Karibu jamii nzima ya kimataifa inasisitiza kuwa hatua ya Israel kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi ni kinyume cha sheria.

3473674/

captcha