IQNA

Matukio ya Palestina

Zaidi ya nusu ya nyumba za Gaza zimebomolewa, Hamas yakanusha madai ya Netanyahu

7:27 - December 12, 2023
Habari ID: 3478026
IQNA- Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imeripoti kwamba asilimia 61 ya nyyumba za raia wa Kipalestina huko Ukanda wa Gaza zimebomolewa katika vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lilolozingirwa.

Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imesema katika taarifa yake kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel hadi sasa limebomoa asilimia 61 ya makazi ya raia wa Palestina katika ukanda huo. Aidha imeelezwa kuwa maghasibu wa Kizayuni wamebomoa nyumba za raia zaidi ya 305,000 katika mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza. 

Taarifa ya Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imeongeza kuwa utawala wa Kizayuni umefanya uharibifu huo katika fremu ya maangamizi ya kizazi ya wananchi madhulumu wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.

Imesema, taasisi za kimataifa zinapasa kutilia maanani suala la kutokea maafa ya binadamu huko Ukanda wa Gaza; kwa sababu kila siku tunashuhudia nyumba nyingi za raia zikibomolewa na kuharibiwa katika eneo hilo. Maghasibu Wazayuni wametumia zaidi ya tani 52,000 za mada za milipuko katika mashambulizi ya kikatili dhidi ya Wapalestina, hospitali, shule na taasisi za kiraia huko Gaza.

Taarifa ya Idara ya Serikali ya Gaza imeeleza kuwa: Wakimbizi milioni moja na nusu wa Kipalestina wanaishi ndani ya Ukanda wa Gaza katika hali ngumu. "Tunashuhudia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza wakati huu wa kuwadia majira ya baridi. Kitendo cha kuzuia bidhaa za chakula na mahitaji mengine muhimu kuingia Ukanda wa Gaza kuna maana ya kutoa hukumu ya kifo kwa raia milioni mbli na laki mbili wa eneo hilo. 

HWakati huo huo msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesisitiza kuwa: Kuuliwa watoto  wa Kipalestina karibu 7,800 huko Gaza ni doa jeusi kwenye paji la uso wa ubinadamu.

Hamas yakanusha uongo wa Netanyahu

Afisa wa ngazi za juu wa harakati ya Hamas amekadhibisha uongo wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu eti kujisalimisha kwa wapiganaji wa harakati hiyo kwa jeshi la Israel akisema uongo huo ni kielelezo cha kufilisika na kushindwa utawala wa Kizayuni kutokana na mapambano makali ya wapigania uhuru wa Palestina.

Ghazi Hamad amesema hayo akikanusha uongo wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni aliyedai kwamba makumi ya wanachama wa Hamas walijisalimisha kwa jeshi la Israel katika siku chache zilizopita na kusema: Hamas kamwe haitakabidhi silaha zake, na wanamapambano hawatajisalimisha, bali watadumisha muqawama.

Hamad ameongeza kuwa: Matamshi yaliyotolewa na Netanyahu na makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni yanaonyesha kuwa licha ya kuwepo tofauti kubwa katika uwezo wa kijeshi wa pande mbili hizo, lakini Wazayuni wako katika mgogoro wa kisaikolojia unaosababishwa na vipigo vya muqawama.

Hamad pia amejibu kauli za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, ambaye ameitaka harakati ya Hamas kusalimu amri na kusema: Unapaswa kuwataka wavamizi wa ardhi ya Palestina wajisalimishe, na sio Hamas!

Afisa huyo wa Hamas amebainisha kuwa, yanayojiri katika medani ya vita ni kielelezo cha wazi kuwa utawala ghasibu wa Israel umeingia kwenye kinamasi ambacho hauwezi kutoka, na serikali ya Marekani pia ni mshirika wa jinai za Israel za kuua raia, kwa sababu inaendelea kuwapa silaha Wazayuni makatili.

Idadi ya majeruhi wa kijeshi wa Israel ni mara tatu ya takwimu rasmi

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limekanusha habari ya jeshi la Israel kuhusu idadi ya majeruhi miongoni mwa wanajeshi wake tangu kuanza vita katika Ukanda wa Gaza, na kuitaja kuwa ni ya uongo kwa kuzingatia kuwa idadi halisi ya majeruhi hao ni mara tatu zaidi ya takwimu rasmi na ripoti zizozotolewa na utawala huo ghasibu.

Haaretz limeongeza kuwa: Tangazo la jeshi la utawala ghasibu wa Israel kwamba wanajeshi 1,593 wamejeruhiwa tangu kuanza vita dhidi ya watu wa Gaza linapingana kwa kiasi kikubwa na idadi ya majeruhi ambayo Haaretz ilipata kutoka hospitalini katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Gazeti hilo limedokeza kuwa idadi halisi ya waliojeruhiwa, kwa mujibu wa vyanzo vya  hospitali 9 za Israel, imeongezeka hadi kufikia askari 4,591.

Tangu tarehe saba mwezi Oktoba, jeshi la Israel limekuwa likitekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa kwa miaka mingi, na hadi sasa raia karibu 19,000 wae eneo hilo wameuawa shahidi na wengine zaidi 48,000 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa watoto na wanawake. Mashambulizi hayo ya Israel pia yamesababisha uharibifu mkubwa pamoja na janga la kibinadamu ambalo kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya Umoja wa Mataifa, halijawahi kutokea.

4187366

Habari zinazohusiana
captcha