IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wa Hija 1444

Umoja na Umaanawi unakabiliwa na uadui na ukwamishaji wa mabeberu

23:00 - June 27, 2023
Habari ID: 3477207
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe muhimu kwa mnasaba wa msimu wa mwaka huu wa Hija akisema, umoja na umaanawi hivi sasa unakabiliwa na uadui na ukwamishaji mkubwa zaidi wa ubeberu, uistikbari na uzayuni.

Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amegusia kwamba, sharti la lazima la kuweza Hijja kuwa na taathira za kimataifa, ni umma wa Kiislamu kuwa na welewa sahihi wa ujumbe muhimu mno uliomo kwenye ibada hiyo ya faradhi chini ya nguzo mbili kuu za umoja na umaanawi. Amesisitiza kuwa: Marekani na kambi nyingine za mabeberu zinapinga vikali kuweko umoja kati ya Waislamu na maelewano kati ya mataifa, nchi na tawala za Waislamu kama ambavyo zinapinga vikali pia kuona vijana wa mataifa ya dunia wanafanya haraka kushikamana na mafundisho ya dini.

Ifuatayo ni matini kamili ya Ujumbe wa Hija wa Ayatullah Khamenei.

 

Bismillahir Rahmanir Rahiim

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na amani na rehema ziwe juu ya Mjumbe Mkuu wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al-Mustafa na kizazi chake kitakatifu na masahaba wake wateule.

Wito wa Hijja wa Nabii Ibrahim (as) na mwaliko wake kwa ulimwengu kwa mara nyingine tena umeuhutubu ulimwengu wote kutoka kwenye moyo wa historia, ukizifanya kuwa na shauku na kuzisisimua nyoyo zilizo tayari na zenye kukumbuka.

Mwaliko huo unaelekezwa kwa wanadamu wote: “Na watangazie watu Hija” (Qur’ani Tukufu 22:27). Al-Kaaba ni mwenyeji aliyebarikiwa na mwongozaji wa watu wote: “Hakika Nyumba ya kwanza waliyowekewa watu kwa ajili ya ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.” (Qur’ani Tukufu 3:96).

Ikiwa ni kitovu na zingatio kuu la Waislamu wote, na pia ibada ya Hija ikiwa ni mfano mdogo wa dhihirisho la pande tofauti za ulimwengu wa Kiislamu, al-Kaaba inaweza kutumika kama chombo kizuri cha kuinua jamii ya wanadamu na kuboresha afya na usalama wa watu wote. Hija inaweza kuwabariki wanadamu wote kwa kuwainua kiroho na kimaadili, na hili ndilo hitajio muhimu la mwanadamu wa leo.

Hijja inaweza kuvunja na kulemaza mipango yote ya madola ya kibeberu yenye kiburi na Uzayuni unaolenga kuharibu na kuporomosha maadili ya binadamu - leo na katika siku zijazo.

Sharti la dharura kwa ajili ya kuthibiti taathira hiyo ya kimataifa ni kwamba kwanza Waislamu wenyewe wanapasa kusikiliza na kuzingatia vizuri ujumbe hai wa Hija na kufanya kila wanaloweza kuutekeleza kivitendo.

Nguzo kuu mbili za ujumbe huo ni "umoja" na "umaanawi." Umoja na umaanawi ndivyo vitu viwili vinavyodhamini maendeleo ya kimaada na kimaanawi ya ulimwengu wa Kiislamu na kuweza kuuangaza ulimwengu mzima. Umoja unamaanisha kuunganika kiakili na kimatendo. Ina maana kwamba nyoyo, mawazo na mielekeo hukaribiana zaidi. Ina maana ya kuwepo ushirikiano katika sayansi na uzoefu, uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi za Kiislamu, uaminifu na ushirikiano kati ya serikali za Kiislamu na kushirikiana dhidi ya maadui wa kawaida na walio wazi. Umoja unamaanisha kwamba njama zilizobuniwa na adui haziwezi kuzigonganisha madhehebu za Kiislamu, mataifa, rangi, lugha, na tamaduni mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu.

Umoja unamaanisha kwamba mataifa ya Kiislamu yanapaswa kufahamiana, si kupitia maelezo na habari za kichochezi za maadui, bali kupitia mawasiliano, mazungumzo na maingiliano. Yanapasa kufahamu suhula na uwezo wa kila mmoja na kupanga mipango ya kufaidika nao.

Umoja una maana kwamba wanasayansi na vyuo vikuu vya ulimwengu wa Kiislamu vinapasa kushirikiana bega kwa bega, wanazuoni na wasomi wa Kiislamu watazamane kwa nia njema, wavumiliane, waamiliane kwa uadilifu na kusikilizana. Wasomi katika nchi zote bila kujali madhehebu zao wawafahamishe watu mambo yanayofanana kati ya Waislamu na kuwahimiza waishi pamoja kwa amani na udugu.

Umoja pia unamaanisha kuwa viongozi wa kisiasa na kitamaduni katika nchi za Kiislamu wanapaswa kujiandaa kwa ajili ya kwenda sambamba na hali itakayojitokeza katika mpangilio ujao wa utawala duniani. Wanahitaji kuamua kwa mikono yao na kwa mapenzi yao wenyewe mahali pazuri pa kuuweka Umma wa Kiislamu katika utawala huo mpya wa kimataifa, ambao umejaa fursa na vitisho. Hawapasi kuruhusu kukaririwa uzoefu mchungu wa uhandisi wa kisiasa na kimaeneo wa Asia Magharibi uliobuniwa na madola ya Magharibi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.

Umaanawi una maana ya kuendeleza maadili ya kidini. Uhamasishaji wa "maadili bila dini," ambao umehamasishwa kwa muda mrefu na wasomi wa Magharibi, umesababisha kuporomoka kusikodhibitika kwa maadili huko Magharibi ambako kila mtu anakushuhudia leo duniani. Watu wanapasa kujifunza umaanawi na maadili kutoka kwenye ibada za Hija, ukawaida uliopo katika vazi la Ihram, kuepuka fursa zisizo za kimantiki kutokana na kauli ya Mwenyzi Mungu inayosema "Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri," na pia "Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija." Tunapasa kujifunza kutokana na amali ya umma mzima kuzunguka mhimili wa Tauhidi, kumpiga mawe shetani [Ibilisi], na kujibari na washirikina (mushrikin).

Ndugu zangu mnaofanya ibada ya Hija! Tumieni fursa iliyojitokeza ya Hijja kwa ajili ya kutafakari na kuzingatia siri na mafumbo ya faradhi hii isiyo na mfano wake na muifanye kuwa masurufu ya maisha yenu yote. Katika wakati na zama hizi, umoja na umaanawi unakabiliwa na uadui na hujuma kali ya madola yenye kiburi na Uzayuni kuliko wakati mwingine wowote. Marekani na vituo vingine vya kiburi ulimwenguni vinapinga vikali umoja wa Waislamu, maelewano kati ya mataifa, nchi na serikali za Kiislamu, dini na kizazi kipya cha vijana kuzingatia thamani za kidini katika mataifa hayo. Wanakabiliana na suala hilo kwa njia na mbinu yoyote wanayoweza. Ni wajibu wetu sote, mataifa na serikali zetu zote kusimama dhidi ya njama hii chafu ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mjuzi na Muweza wa yote, aimarishe moyo wa kujibari na washirikina ndani yenu, na mtambue kwamba mna jukumu la kueneza na kuimarisha moyo huo kwenye mazingira mnayoishi.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie nyinyi nyote Mahujaji wa Kiirani na wasio Wairani, mafanikio na Hijja yenye kukubaliwa na yenye baraka. Ninamwomba awatakabalie dua zenu nyote kwa baraka na utukufu wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (af), roho zetu ziwe fidia kwake.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi wa Barakatuh.

 

Seyyed Ali Khamenei

Dhu al-Hijja 6, 1444

Juni 25, 2023

captcha