IQNA

Mbinu ya Elimu ya Manabii; Ibrahim/1

Kuelimisha kwa kuelezea matokeo ya kitendo

17:11 - May 29, 2023
Habari ID: 3477065
TEHRAN (IQNA) – Katika kuwaelimisha watu wake, Nabii Ibrahim (AS) alijaribu kwanza kuwaonyesha matokeo ya matendo yao yatakavyokuwa.

Katika ulimwengu wa leo wakati maendeleo ya teknolojia yameathiri mienendo na tabia ya watu, kujifunza kuhusu mbinu za elimu au kuwaelimisha wengine zinazoweza kusababisha uboreshaji wa tabia katika ngazi ya mtu binafsi na kijamii ni muhimu sana.

Njia moja ya kielimu ambayo kwa kawaida hutumiwa na wazazi na walimu ni kuwajulisha watoto matokeo ya matendo yao. Inatekelezwa kwa njia mbili:

Katika ya kwanza, mwalimu anamwambia mtoto kuhusu kile kitakachotokea kutokana na kile anachofanya bila kudhoofisha kujiheshimu kwake au kumfanya afadhaike.

Katika njia ya pili, mwalimu anamkataza mtoto kufanya kitu na kisha kumruhusu kukabiliana na matokeo ya matendo yake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatumia njia hii kuwafundisha wanadamu. Mtu anapokumbana na msiba huwa anashangaa kwa nini amedhulumiwa lakini ukweli ni kwamba ni matokeo ya matendo yake mwenyewe. “Jema lilio kufikia limetokana na Mwenyezi Mungu. Na ovu lilio kusibu linatokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kutosha.” (Aya ya 79 ya Surah An-Nisa)

Ndiyo maana Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 33 ya Surat An-Nahl: “Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali walijidhulumu nafsi zao."

Nabii Ibrahim (AS) ni Ulul Adhm yaani ni miongoni wajumbe wa Mwenyezi Mungu ambaye jina lake limetajwa katika aya nyingi za Qur'ani Tukufu. Yeye, pia, alitumia njia hii ya elimu. Ili kuwafahamisha makafiri matokeo ya matendo yao, alisema: “Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua?" (Aya ya 81 ya Surah Al-Anaam)

Kwa hakika, Nabii Ibrahim (AS) anawataja makafiri kwenye kitendawili chao cha ndani, akisema: “Mnanionya juu ya yale ambayo hayatakiwi kuogopwa na nyinyi wenyewe hamuogopi mnachopaswa kukiogopa.

Anawaonya kwamba wakiendelea kutembea kwenye njia ya Shirki (ushirikina), watakumbana na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

captcha