IQNA

Serikali ya Iraq yakosolewa kwa kumkamata kamanda wa Hashd Al Shaabi

18:52 - May 28, 2021
Habari ID: 3473955
TEHRAN (IQNA)- Mwenyekiti wa Muungano wa Fath nchini Iraq amesema Jeshi la Kujitolea la Wananchi Iraq, maarufu kama Hashd al Shaabi (PMU), kwa damu yake toharifu limeweza kuipa nguvu serikali ya Iraq na hivyo kila ambaye anataka kusamabratisha nguvu na uwezo wa jeshi hilo kimsingi atakuwa amedhoofisha nguvu za taifa la Iraq.

Al Amiri  Mwenyekiti wa Muungano wa Fath ametoa tamko hilo Ijumaa kufuatia kukamatwa Qasim Muslih Kamanda wa Hashd al Shaabi nchini Iraq katika mkoa wa Al Anbar.

Katika taarifa hiyo, Al Amiri amesisitiza kuwa, kupuuzwa vyombo vya mahakama na sheria ni hatua moja katika kuelekea udikteta.

Qasim Muslih alikamatwa Jumatano kufuatia mashinikizo ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad na punde baada ya kamanda huyo kutiwa mbaroni kumeshuhudiwa wimbi la malalamiko kutoka makundi mbali mbali ya kisiasa na muqawama nchini Iraq.

Kamanda Qasim Muslih,  ni miongoni mwa makamanda wenye nafasi muhimu sana katika kukabiliana na magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh nchini Iraq. Wakati akikamatwa alikuwa anasimamia oparesheni za kuwasaka magaidi wa ISIS walio mafichoni katika mkoa la Al Anbar.

Aidha Muslih amezuia misafara ya wanajeshi wa Marekani kuingia Iraq kinyume cha sheria kupitia mpaka wa Al Anbar. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa kukamatwa Qasim Muslih kunatokana na kitendo chake cha kuzuia msafara wa Wamarekani kuingia Iraq kinyume cha sheria.

3974115

captcha