IQNA

Waliofika fainali mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran watangazwa

18:14 - January 26, 2021
Habari ID: 3473593
TEHRAN (IQNA)- Waliofika fainali katika Mashindano ya 37 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran wametangazwa na kamati andalizi.

Kwa mujibu wa kamati hiyo wasomaji Qur'ani (quraa) kutoka  Indonesia, Iran, Iraq, Syria, Misri, na Lebanon  watashindano katika fainali ya kategoria ya Tahqiq huku katika kategoria ya Tarteel waliofika fainali wakiwa ni kutoka  Misri, Iran, Indonesia, Iraq, Algeria, Syria na Uholanzi.

Waliofika katika fainali katika kategoria ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilkifu ni kutoka Afrika Kusini, Russia, Afghanistan, Iran, Iraq, Marekani, Mauritania na Libya.

Aidha mbali na mashindano hayo ya kawaida kutakuwa na fainali za mashindano maalumu ya Qur'ani kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya kidini na wanawake.

Majaji Wairani katika mashindano hayo walikuwa katika ukumbi wa Shirika la Wakfu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku majaji wa kigeni wakishiriki kwa njia ya intaneti kutoka Syria, Sudan, Iraq, Lebanon na Indonesia.

Fainali za mashindano hayo zinatazamiwa kufanyika mapema mwezi Machi kwa mnasaba wa Idi ya Mab'ath ambayo huwa siku ya kusherehekehea kuanza Utume wa Mtume Muhammad SAW.

Semi fainali ya mashindano hayo imefanyika mapema mwezi huu kwa njia ya intaneti ambapo kulikuwa na washiriki 120 kutoka nchi 70. Duru za awali za mchujo katika mashindano hayo zilikuwa na washiriki 600 kutoka nchi 70 na zilifanyika pia kwa njia ya intaneti kutokana na janga la corona.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani kila mwaka.

Kutokana na janga la COVID-19 mashindano hayo hayakufanyika mwaka 2020 na yalifanyika mara ya mwisho Aprili 2019 mjini Tehran ambapo washiriki kutoka nchi zaidi ya 80 walishiriki.

3949998

captcha