Kwa mujibu wa Jarida la Vice, mtandao wa madalali wa data umeuganisha aplikesheni hiyo na taasisi za kiusalama za Marekani kama vile ICE na FBI. ICE ni Kikosi Maalumu cha Mamlaka ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani nayo FBI ni Idara ya Upelelezi ya Marekani ambayo kimsingi ni taasisi kuu ya ujasusi na usalama wa ndani nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa aplikeshni hiyo ambayo inajulikana kama Salaat First iliundwa ili kuwasaidia Waislamu kutekeleza faradhi ya swala za kila siku ambapo huwakumbusha wakati wa swala na kubaini muelekeo wa Qibla huku ikiwa pia na uwezo kutambua misikiti iliyokaribu. Aplikesheni hiyo inahitaji mtumizi kuwasha mfumo wa GPS au location data kubaini aliko.
Kwa mujibu wa taarifa, aplikesheni hiyo imekuwa ikiuza taarifa za watumizi kwa shirika moja la Ufaransa liitwalo Predicio, ambalo kimsingi hufanya kazi za udalali kuuza taarifa za watumizi kwa wanaozitaka. Mashirika ya usalama ya Marekani ambayo hununua taarifa za watumizi kutoka Predicio ni pamoja na FBI na ICE. Aplikesheni hiyo ya Salaat First ina watumizi zaidi ya milioni 10. Hivi karibuni pia jarida la Vice lilifichua namna ambavyo aplikesheni ya Muslim Pro, yenye watumizi zaidi ya milioni 100 imekuwa ikiuzia Jeshi la Marekani taarifa za watumizi Waislamu.