IQNA

Waziri Mkuu wa Morocco apinga uhusiano na Israel

14:43 - August 24, 2020
Habari ID: 3473098
TEHRAN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Morocco Saad Eddine El Othman amesema nchi yake inapinga kuanzisha uhusiano wowote na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akihutubu mbele ya chama chake cha Kiislamu cha PJD, El Othmani amesema: "Tunapinga uanzishwaji uhusiano na utawala wa Kizayuni kwa sababu hatua kama hiyo itaupa kiburi zaidi kuendelea kukiuka haki za Wapalestina."

Morocco imekuwa ikiunga mkono suluhisho la mgogoro wa Palestina kwa kuzingatia kile kinachotajwa kuwa ni 'suluhisho la nchi mbili' huku Quds (Jerusalem) Mashariki ukiwa mji mkuu wa taifa la Palestina.

Morocco na Israel zilianzisha uhusiano wa kiwango cha chini mwaka 1993 baada ya kutiwa saini mapatano ya amani baina ya Palestina na Israel. Hata hivyo baada ya mwamko wa Wapalestina mwaka 2000, Rabat ilisimamisha uhusiano wake huo na utawala wa Kizayuni.

Marekani imedai kuwa katika miezi ijayo, nchi kadhaa za Kiarabu zitaanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)  na utawala haramu wa Kizayuni, tarehe 13 Agosti pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Makubaliano hayo kati ya Israel na UAE  yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu na shakhsia kadhaa wa kisiasa duniani, ambao karibu wote wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, hatua hiyo ya UAE ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

3472363

captcha