IQNA

Al Azhar yampongeza Papa Francis kwa kulaani mauaji ya Waislamu Myanmar

23:27 - February 11, 2017
Habari ID: 3470843
IQNA-Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimempongeza Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis kwa msimamo wake wa kulaani mauaji na ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar.

Siku ya Jumatano, Papa Francis, alisema kwamba Waislamu wa Myanmar wananyanyaswa kwa miaka mingi sasa na wanauawa na kuteswa kinyama kwa sababu tu ya kutaka waishi kwa mujibu wa utamaduni na mafundisho ya dini yao. 

Akizungumza katika makao ya Kanisa Katoloki Duniani mjini Vatican, Papa Francis alisisitiza kuwa, kuna wajibu wa kutetewa haki za Waislamu wa Rohingya na kuzuia kufukuzwa Myanmar Waislamu hao na kupelekwa nchi nyingine.

Al Azhar imetoa taarifa na kusema msimamo huo wa Papa ni ishara kuwa nafahamu vyema masuala ya kimataifa. Aidha Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni ISESCO nalo pia limempongeza papa kwa mtazamo wake huo na kueleleza matumaini kuwa msimamo huo utatoa msukumo kwa jamii ya kimataifa kuhitimisha ukandamizaji wa Waislamu Myanmar.

Hayo yanajiri  katika hali ambayo Umoja wa Mataifa umetoa ripoti na kuthibitisha kuwa, askari wa Myanmar wamefanya jinai na mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa kaskazini mwa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwanajisi wanawake kwa makundi na kuchoma moto vijiji vya Waislamu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema, askari wa serikali ya Myanmar hawakuwahurumia hata watoto wachanga, watoto wadogo, wanawake na wala vizee wakati walipofanya opereseheni za kuwafyatulia risasi kiholela raia Waislamu na kuchoma vijiji vyao.

Tangu mwezi Oktoba 2016, jeshi la Myanmar lilianzisha operesheni maalumu ya mauaji ya kizazi cha Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhime, la kaskazini mwa nchi hiyo.

3462179

captcha