IQNA

Wazayuni waushambulia Msikiti Ukingo wa Magharibi

5:00 - November 29, 2015
Habari ID: 3457989
Wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel wameendeleza hujuma zao za kidhalimu dhidi ya Wapalestina kwa kuuhujumu Msikiti katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Duru za habari zimedokeza kuwa msikiti uliohujumiwa uko katika eneo la Beit al Amr kaskazini mwa Al Khalil katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwingineko askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewajeruhi kwa kuwapiga risasi makumi ya Wapalestina katika mashambulio waliyofanya katika maeneo kadhaa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limetangaza leo kuwa Wapalestina wasiopungua 24 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi wakati askari wa utawala haramu wa Israel walipovamia kambi ya Al-Arub na kitongoji cha Halhul huko Al- Khalil katika Ufukwe wa Magharibi. Katika tukio jengine, Wapalestina zaidi ya 50 wamejeruhiwa baada ya kuvuta gesi ya sumu wakati askari wa utawala ghasibu wa Kizayuni walipowatawanya Wapalestina na kuwashambulia kwa gesi ya kutoa machozi na mabomu ya sauti. Wapalestina wengine wasiopungua 16 wamejeruhiwa wakati askari wa Kizayuni waliposhambulia mji wa Nablus katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. Katika upande mwengine, manowari ndogo za jeshi la utawala wa Kizayuni zimewashambulia wavuvi wa Kipalestina katika maji ya Ukanda wa Gaza. Aidha Wapalestina wasiopungua 26 wamejeruhiwa katika mapigano kati yao na askari wa Kziayuni yaliyotokea kwenye maeneo ya mpaka wa pamoja wa Ukanda wa Gaza na yale yaliyopewa jina la Israel. Kwa mujibu wa takwimu za kituo cha Taaluma za Masuala ya Israel na Palestina cha Quds, tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba hadi sasa, askari wa utawala wa Kizayuni wamewaua shahidi Wapalestina 104 wakiwemo watoto wadogo na chipukizi 22 na kuwajeruhi wengine zaidi ya elfu mbili.

3457831

captcha