IQNA

Mkutano wa 28 wa Kimatiafa wa Umoja wa Kiislamu waanza Tehran

20:46 - January 07, 2015
Habari ID: 2684304
Mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu.

Katika ufunguzi wa mkutano huo Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa Siku ya Kuzaliwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) na Imam Jaafar Swadiq (A.S), amesema kwamba, ili kuimarisha umoja katika ulimwengu wa Kiislamu inapasa kuondolewa mambo yanayozusha migongano, kuainisha vitisho vya pamoja vya ulimwengu wa Kiislamu na  watu wote kubainishiwa vitisho hivyo. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesisitiza juu ya ushirikiano katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuimarisha umoja na pia kutambuliwa madhehebu zote kama matawi ya dini.  Rais Rouhani pia ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kuungana kivitendo. Huku akiashiria mauaji na matukio ya kustaajabisha yaliyojiri mwaka uliopita katika nchi za Kiislamu, Dakta Rouhani amesema kuwa, umoja wa Kiislamu hautopatikana katika ulimwengu wa  Kiislamu kwa kukaririwa maneno matupu ya umoja na kufanyika mikutano ya kuhamasisha umoja, bali kwamba hatua hizo zinaweza kuwa mwanzo wa kuelekea katika njia iliyo ngumu ya keleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu.  Muhsin Araki Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu naye pia katika ufunguzi wa mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu amewataka viongozi wa nchi za Kiislamu badala ya kuamiliana kwa uadui, wakurubishe mioyo ya Waislamu kwa tadbiri na kutumia muongozo wa Qur'ani Tukufu.  Pia amewataka viongozi wote wa nchi za Kiislamu na shakhshia wenye nafasi katika ulimwengu wa Kiislamu kufanya jitihada za kuimarisha umoja hasa katika nchi ambazo sasa zinashuhudia migogoro. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ameongeza kwamba, katika kipindi ambacho mwamko wa Kiislamu umehuisha tena utambulisho wa Kiislamu, makundi maovu na yaliyopotoka ambayo nyuma yao kuna maadui wa Uislamu, hayajaweza kuvumilia hali hiyo na kwamba yanafanya njama za kuwatenganisha Waislamu kwa njia tofauti.

Naye Sheikh Naem Qassim Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya utumiaji mabavu wa Marekani na kusema kwamba, msimamo huo wa Iran wa kupinga hatua ya Marekani ya kuvamia Afghanistan na Iraq na pia Israel kukalia kwa mabavu Israel ardhi za Wapalestina unapaswa kuimarishwa. Sheikh Qassim ameongeza kuwa, Hizbullah inakabiliana na Israel, makundi ya kitakfiri na mpango wa Israel wenye  lengo la kutawala eneo la Mashariki ya Kati.  Katika mkutano huo kumefanyika maonyesho ya jumla ya vitabu 63 vya hadithi za pamoja za Shia na Sunni, na pia kuenziwa maulamaa kama vile Imam Mussa Sadr, Ayatullah Waedhzadeh na Allama Shikeh Said Shaaban mmoja wa shakhsia wa Kisunni wa nchini Lebanon. Imam Khomeini (M.A) Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu alitangaza tarehe 12 hadi 17 ya Rabiul Awwal ambazo ni tarehe za maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Mtukufu (SAW) kwa mujibu wa riwaya za Sunni na Shia kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Kwa mnasaba huo, katika kipindi hicho Waislamu wote wa madhehebu ya Sunni na Shia nchini Iran hufanya sherehe na hafla za kuadhimisha wiki ya umoja.../mh

2681894

captcha