IQNA

Jinai za Israel

Ayatullah Khamenei: Israel ilipata kipigo katika Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa

19:07 - November 22, 2023
Habari ID: 3477929
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema utawala haramu wa Israel "iliangushwa" katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, operesheni kubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina dhidi ya utawala huo ghasibu.

Ayatullah Khamenei amesema hayo jijini Tehran leo alipokutana na kundi la wanamichezo wa Iran na washindi wa medali walioshiriki katika Michezo ya Asia ya mwaka 2023 huko Hangzhou, China.

Akizungumza Jumatano, Kiongozi Muadhamu amesema: " Ikiwa nitakupa mchanganuo juu ya matukio ya hivi karibuni, ni kwamba,  utawala wa Kizayuni uliangushwa katika Operesheni ya Kimbung cha Al-Aqsa."

"(Harakati ya muqawama wa Palestina) Hamas, sio kama serikali na nchi yenye suhula za kutosha, bali kama kundi la wapiganaji, ambalo liliweza kutoa pigo la mtoano na la mwisho kwa Wazayuni maghasibu wenye kila aina ya zana."

Ayatullah Khamenei amewapongeza wanamichezo hao ambao walionyesha uungaji mkono wao kwa Palestina na kadhia ya Palestina, na kujiondoa katika mashindano na wawakilishi wa utawala ghasibu wa Israel katika mashindano ya kimataifa ya michezo ya Hangzhou, akisema ukweli wa kitendo chao sasa unadhihirika zaidi kuliko wakati mwingine wowote baada ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Leo, dunia nzima imetambua kwa nini mwanariadha wa Iran hatakubali kukabiliana na upande wa Kizayuni uwanjani. Hii ni kwa sababu [mwanariadha wa Kizayuni] ni mhalifu na anafanya michezo na kwenda uwanjani kwa niaba ya utawala unaotenda jinai na kwa hivyo anaisaidia serikali ya kigaidi na uhalifu.”

Huku akisisitiza kuwa utawala wa Israel bado unaendelea kulemewa na mzigo na fedheha ya kushindwa vibaya baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, Kiongozi Muadhamu amesema, “Ndio, wanatanua misuli yao; lakini wapi? Onyesho hili la nguvu halina thamani inapokuja kwa hospitali za wagonjwa huko Gaza, kwa shule za Gaza, juu ya vichwa vya watu wasio na makazi wa Gaza".

Ayatollah Khamenei ameongeza kuwa, "Ni kana kwamba mwanariadha anashindwa uwanjani, na kisha kulipiza kisasi kwa hasara hiyo, anawashambulia mashabiki wa timu pinzani, kuwatukana na kuwapiga."

Akiashiria mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Gaza katika kipindi cha siku 47 zilizopita, Kiongozi Muadhamu amesema: "Hakuna jambo la kufedhehesha zaidi kuliko yale ambayo utawala wa Kizayuni umeyafanya. Kushindwa kubaya utawala wa Kizayuni hakutafidiwa na milipuko hii ya mabomu; kampeni kama hizo za mabomu zitafupisha tu maisha ya utawala huu ghasibu na ubabe na ukatili huu hautapita bila kujibiwa.”

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelaani kuingizwa siasa katika michezo na undumakuwili wa baadhi ya taasisi za kimataifa.

Amebaini kuwa:  "Wanasema michezo si ya kisiasa, lakini wanapohitaji kuingiza siasa kwenye michezo, wanaiingiza katika hali mbaya zaidi. Kwa kisingizio kidogo, nchi imepigwa marufuku kushiriki katika hafla zote za kimataifa za michezo. Kwa nini? [Kwa sababu] ilipigana mahali fulani; lakini wao wenyewe, wanapuuza watoto 5,000 waliouawa kishahidi huko Gaza.”

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa wanapiga marufuku nchi kwa kisingizio cha vita huku wakipuuza vita vya nchi nyingine, uhalifu wa kivita na hata mauaji ya halaiki.

4183469

Habari zinazohusiana
captcha