IQNA

WFP: Weyemen milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

19:55 - December 04, 2020
Habari ID: 3473420
TEHRAN (IQNA) - Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa indhari kuhusu uwezekano wa mamilioni ya watu wa Yemen kupoteza maisha kutokana na njaa huku Saudi Arabia ikiendeleza vita dhidi ya nchi hiyo masikini zaidi ya Kiarabu.

Katika taarifa WFP, imesema tathmini zinaonyesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021, watu milioni  tano hawatakuwa na uwezo wa kupata chakula nchini Yemen.

Aidha uchunguzi umebaini kuwa kati ya Januari na Juni 2021, asilimia 54 ya Wayemen, yaani watu milioni 16.2, watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Mkurugenzi wa WFP David Beasley amesema takwimu hizo zinapaswa kuamsha hisia za jamii ya kimataifa ili kuzisaidia mamilioni ya familia nchini Yemen.

Hayo yanajiri wakati ambao, Jumatano  wakuu wa Yemen walitoa tahadhari kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya nchini humo kutokana na vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu ambapo 'mtoto mmoja wa Yemen hupoteza maisha kila dakika 10'.

Aidha Jumanne pia Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

3473305

Kishikizo: yemen mtoto njaa vita saudia
captcha