IQNA

Jeshi la Nigeria labomoa kabisa ukumbi wa Waislamu

23:13 - December 21, 2015
Habari ID: 3467977
Jeshi la Nigeria limetumia buldoza kubomoa kikamilifu ukumbi wa Husseiniyyah Baqiyyatullah katika mji wa Zaria sehemu ambayo ni makao makuu ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, Husseiniyah hiyo ambayo ni makao makuu ya harakati za Kiislamu za Mashia katika mji wa Zaria imebomolewa kikamilifu na jeshi la Nigeria na kusawazishwa na udongo.

Hatua hiyo ya jeshi la Nigeria inachukuliwa katika hali ambayo, mauaji ya kinyama ya jeshi hilo ya juma lililopita yameendelea kulaaniwa katika kila kona ya dunia huku serikali ya nchi hiyo ikitakiwa kuwachukulia hatua waliohusika na jinai hiyo.

Wakati huo huo maafisa wa Nigeria wamesema kuwa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na wafuasi wake watapandishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka.

Wiki iliyopita jeshi la Nigeria liliishambulia Husseiniyyah ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria pamoja na nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuwaua mamia ya Waislamu kwa kisingizio kwamba Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikula njama ya kutaka kumuua kamanda wa jeshi na kufunga njia kwa ajili ya shughuli za mijumuiko ya harakati hiyo. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, idadi ya waliouawa katika shambulio hilo la jeshi la Nigeria inafikia elfu moja.

3467819

captcha