IQNA

Shirika la ICRO lalaani mauaji ya Mashia Nigeria

21:43 - December 17, 2015
Habari ID: 3464304
Shirika la Iran la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu ICRO limetoa taarifa na kulaani hujuma ya hivi karibuni ya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ambapo zaidi ya waumini 1000 wameripotiwa kuuawa.

Katika taarifa, ICRO imeitaja hujuma ya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu Mashia nchini humo kuwa ni hujuma ya kinyama na kwamba hiyo ni njama ya kuonesyha kuwa nchi za Waislamu hazina usalama na uthabiti.
"Katika nchi ambayo,  kundi la Boko Haram, muitifaki wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh, linahujumu ustaarabu na ubinadamu sambamba na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya watu wa Nigeria, ni vipi jeshi linaweza kuhalalisha hujuma ya kinyama dhidi ya jamii ya watu wapendao amani na kuwaua kwa umati watu wasio na hatia,?" imehoji taarifa hiyo ya ICRO.
Shirika la Iran la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu ICRO limetoa wito kwa taasisi za kimataifa na Kiislamu kuchukua msimamao imara dhidi ya kitendo hicho kilicho dhidi ya ubinadamu na Uislamu ili kuzuia kururdiwa tena maafa kama hayo.
Ikumbukwe kuwa, kwa kutoa tuhuma kwamba Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikula njama ya kutaka kumuua kamanda wa jeshi na kufunga njia kwa ajili ya shughuli za mijumuiko ya harakati hiyo, Jumamosi iliyopita, jeshi la Nigeria liliishambulia Husainiyyah ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria na siku ya Jumapili likahujumu nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuwaua mamia ya Waislamu.
Kuhusu idadi ya watu waliouawa, Nusaibah Zakzaky, binti wa Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema watu wapatao 450 waliuawa huko Zaria na maiti zipatazo 300 ziko hospitalini, na hivyo idadi kamili ya waliouawa inaweza kufikia watu 1000.
Kwingineko Wanaharakati wa Nigeria wameripoti kuwa maiti za Waislamu waliouawa katika maafa ya Zaria kaskazini mwa nchi hiyo zinachomwa moto na kuzikwa kwenye makaburi ya halaiki.
Wanaharakati hao wamefafanua kuwa serikali na jeshi la Nigeria zimezika maiti za Waislamu kwenye makaburi ya halaiki na kuzichoma moto baadhi ya nyengine ili kufuta ushahidi wa jinai ziliyotenda katika maafa ya Zaria.
Wanaharakati hao wamefafanua kuwa haifahamiki idadi hasa ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliouliwa kwa umati na jeshi la nchi hiyo; na kwa sababu hiyo jeshi hilo linajaribu kufuta kila kielelezo na ushahidi uliopo ili ukubwa wa jinai lililotenda usiweze kujulikana.

3464037

captcha