IQNA – Msomi mmoja kutoka chuo kikuu cha Lebanon amesema kuwa maadili ya Kiislamu kuelekea wasio Waislamu yamejengwa juu ya msingi kwamba wanadamu ni ama ndugu zako katika dini au wako sawa na wewe katika uumbaji.
Sheikh Ahmed Qattan, msomi wa Kisunni kutoka Lebanon na mkuu wa jumuiya ya ‘Quluna wa al-Amal’, ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) wakati Waislamu wakijawa na huzuni kwa mnasaba wa 28 Safar, ambayo ni siku ya kukumbuka kifo cha Mtume Muhammad (SAW). Alibainisha kuwa maisha ya Mtume Mtukufu (SAW), kabla na baada ya kupewa utume, yalikuwa mfano bora wa kuponya migawanyiko na kuimarisha umoja, kuanzia kusuluhisha mzozo wa kuwekwa kwa Hajar al-Aswad (Jiwe Jeusi) na kuokoa damu za makabila ya Makka, hadi wito wa kuishi kwa amani na wafuasi wa dini nyingine.
Yafuatayo ni maelezo mafupi kutoka kwa hotuba yake wakati wa mahojiano hayo:
"Kila tunapotaka kuzungumzia maisha ya Mtume Muhammad (SAW), hususan tunaposhughulika na wasio Waislamu, tunaanza na kauli hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Enyi wanadamu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke, na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takwa zaidi kati yenu.’ (Surah Al-Hujurat: 13)
Hivyo, dini yetu ya Kiislamu inawatendea wasio Waislamu kwa msingi kwamba wanadamu ni wa aina mbili: ama ni ndugu zako katika dini, au ni sawa na wewe katika uumbaji, kama alivyosema bwana wetu Imam Ali bin Abi Talib (AS). Na ni wajibu kwetu kuwatendea wasio Waislamu kwa namna inayoakisi Uislamu wetu na maadili yetu, ambayo yalitokana na kumfuata Mtume wetu Muhammad (SAW).
Kwa hiyo, tunawatendea hata wasio Waislamu, Wakristo na Wayahudi, kwa maadili yetu thabiti na tunaepuka tabia yoyote inayochangia taswira mbaya ya Uislamu wetu tunaoupenda.
Kuhusu hatua alizochukua Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuanzisha umoja na undugu kati ya mataifa na makabila tofauti, ni lazima kusema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) daima alikuwa akitafuta kuziba mapengo na kuunganisha safu za watu, hata kabla ya utume. Sote tunajua kuwa kabla ya utume, wazee wa Makka walipokuwa wakitaka kuweka Hajar al-Aswad, walisema watamfanya mtu wa kwanza kuingia hapo awe mwamuzi. Walipoona kuwa ni Muhammad (SAW) ameingia, walimkubali kama mwamuzi wao. Ili kuzuia mgogoro na kutoelewana, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliwaambia kila kabila lishike pembe ya nguo, kisha yeye akaweka Hajar al-Aswad katikati ya nguo hiyo na kuiweka katika nafasi yake maalumu kwa mkono wake mtukufu. Kwa njia hiyo, aliokoa damu za wale waliokuwa wakipigana kuhusu kuwekwa kwa Hajar al-Aswad. Baada ya utume kuanza, daima alitafuta kuponya migawanyiko kati ya watu, kwa sababu yeye ni nabii na mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na anatakia kheri kila mtu.
Kuhusu mkataba wa undugu uliotiwa saini kati ya Waislamu wa Ansar na Muhajirin, ni jambo la kawaida kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alianzisha mkataba wa undugu kati yao alipoingia Madina, na undugu huo ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba uliimarisha maisha ya undugu wa Waislamu, kwa namna ambayo sote ni Ummah mmoja.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa daima akijitahidi katika viwango vyote vya kiuchumi na kijamii. Ikiwa hii inaashiria jambo lolote, ni kwamba hakuwa mtu wa kawaida, bali alikuwa nabii na mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Daima aliwashauri Waislamu kutafuta elimu na kuongeza maarifa yao, kwa sababu aya ya kwanza iliyoteremshwa katika moyo wake mtukufu ilikuwa neno Iqra, yaani ‘Soma’.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema: ‘Malaika hutandika mbawa zao kwa ajili ya mtafuta elimu kutokana na radhi ya kile wanachokisikia.’ Alikuwa daima akihimiza kutafuta elimu na kusema: ‘Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu, mwanamume na mwanamke.’ Ikiwa hii inaashiria lolote, haionyeshi kitu kingine isipokuwa shauku yake kubwa na maslahi yake katika elimu na ufahamu wake wa thamani yake."
3498622