IQNA

Allamah Tabatabai alifungua njia mpya ya tafsiri ya Qur'ani

17:39 - May 12, 2022
Habari ID: 3475242
TEHRAN (IQNA) – Mwanachuoni wa kidini alisema Allamah Seyed Mohammad Hossein Tabatabaei alifungua njia mpya katika tafsiri ya Kurani Tukufu.

Ayatullah Ahmad Mobaleghi alisema njia hii iliimarisha mafungamano kati ya Qur'ani Tukufu na jamii.

Alisikitika kwamba njia hii haikuendelea baada ya Allameh Tabatabaei, akisema inapaswa kutekelezwa na kuundwa maendeleo ya kimsingi katika masomo ya tafsiri.

Ayatullah Mobaleghi amesisitiza kuwa, utafiti wa kidini ni muhimu sana katika utendaji wa dini na kusema, iwapo dini itakuwa msingi wa jamii na serikali, inahitaji mbawa mbili za imani na fikra za kidini.

Ameongeza kuwa matatizo mengi yanayoikabili jamii hivi leo yanatokana na umakini mdogo unaotolewa kwa masuala ya dini na masomo ya kidini.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alisema utafiti na uchunguzi kuhusu imani ya watu na fikra za kidini zinapaswa kuendelea ili kubaini matatizo na njia za kuimarisha imani katika jamii.

Ameashiria aya ya 13 ya Sura Ash-Shura (42), “Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye,” na kuongeza kuwa dini ndio msingi na nguzo ya kusonga mbele.

Amesema ili kunufaika na Qur'ani Tukufu katika kutatua masuala ya leo, kuna haja ya tafsiri sahihi na kwamba nayo inahitaji mabadiliko ya kimsingi katika masomo ya Tafsiri ya Qur'ani Tukufu.

Ayatullah Mobaleghi ameongeza kuwa, kufaidika na Qur'ani kunahitaji masomo ya kina zaidi na kufuata njia iliyofunguliwa na Allamah Tabatabei.

Allamah Seyed Mohammad Hussein Tabatabai, (Machi 1903 – Novemba 1981) alikuwa mmoja wa wanafikra mashuhuri katika Uislamu wa kisasa wa Shia.

Anajulikana sana kwa Tafsir Al-Mizan, yenye juzuu ishirini na saba  za Tafsiri ya  Qur'ani aliyo kati ya 1954 na 1972.

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai alikuwa mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani na tafsiri yake ya Qur’ani ya al Mizan ilikuwa ya aina yake. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini zaidi za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.

Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa katika lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiswahili, Kiingereza, Kihispania.

3478863

captcha