IQNA

Bibi Fatima Zahra SA katika Qur’ani Tukufu

13:05 - January 17, 2021
Habari ID: 3473564
TEHRAN (IQNA)- Siku kama ya leo miaka 1431 iliyopita, yaani tarehe 3 Jumada Thani mwaka wa 11 hijria, Bibi Fatima Zahra Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu Yake- Salamullah Alayha- (SA), binti kipenzi cha Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa Imam Ali bin Abi Talib SA alikufa shahidi baada ya kuishi umri mfupi tu lakini uliojaa baraka.

Aidha kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra alikufa shahidi tarehe 13 Jamadil Awwal.

Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo wa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Talib AS na maswahaba wengine wa Mtume alisifika mno kwa tabia njema, uchamungu na elimu. Aa alikuwa mfano na kiigizo chema cha Waislamu. Bibi huyu alikuwa na nafasi aali na ya juu sana kiasi kwamba, Mtume Muhammad SAW amemtaja kuwa ni mbora wa wanawake wote duniani. Si hayo tu bali wafasiri wa Qur'ani tukufu wanasema kuwa, Mwenyezi Mungu SW amemkirimu sana mja wake huyo mwema na familia yake kwa kuteremsha sura nzima ya Qu'ani iliyopewa jina la al Kauthar. Vilevile Mwenyezi Mungu SW ameenzi na kubakisha hai kujitolea kwa Fatima na familia yake katika aya kadhaa za Suratul Insan na kutaja sifa na matukufu yake mengi katika aya nyingine nyingi za Qur'ani tukufu.

Hakika tumekupa kheri nyingi

Bibi Fatimatu Zahraa ni mwana wa Mtume Muhammad SAW na Bibi Khadija binti Khuwailid. Bibi Khadija alimzalia Mtume mtoto wa kiume aliyepewa jina la Abdullah lakini baada ya muda si mrefu, mtoto huyo alifariki dunia. Baada ya tukio hilo mmoja kati ya vinara wa washirikina wa Makka aliyejulikana kwa jina la al A's bin Wail alikutana na Mtume SAW akitoka katika Masjidul Haram na kuzungumza naye. Kundi moja la vinara wa kabila la Quraish ambao waliona mazungumzo hayo yakifanyika walimsubiri al A's hadi alipoingia katika Msikiti wa Makka na kumuuliza: Ulikuwa ukizungumza na nani? na yule Abtar aliyekatikiwa na kizazi? Ni wakati huo ndipo Mwenyezi Mungu SW alipoingilia kati ya kumtetea Mtume wake kwa kuteremsha Suratul Kauthar inayosema:  Hakika tumekupa kheri nyingi. Basi sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi. Hakika mwenye kukubughudhi ndiye aliyekatikiwa na (kizazi). “

Wafasiri wa Qur'ani tukufu wanasema al Kauthar ina maana ya kheri na baraka nyingi. Wanasema makusudi ya kheri hiyo ambayo Mwenyezi Mungu SW amemtunuku Mtume wake wa mwisho, Muhammad (saw) ni kukithirisha kizazi chake, suala ambalo lilitimia kupitia kwa binti yake kipenzi, Fatimatu Zahra AS. Kwa kadiri kwamba, kizazi chake sasa hakihesabiki kwa wingi wake katika pembe mbalimbali za dunia na hali hiyo itaendelea mpaka Siku ya Kiyama. Kheri hii aliyopewa Mtume ilikuwa jibu kwa washirikina wa Makka waliokuwa wakimbughudhi Mtume SAW kwamba, amekatikiwa na kizazi baada ya kufariki dunia watoto wake wote wa kiume.

Baadhi ya maulama wa Kiislamu pia wanasema Bibi Fatumatu Zahra AS mwenyewe ndio kielelezo kikubwa na cha wazi zaidi cha hiyo kheri nyingi yaani (al Kauthar) aliyopewa Mtume Muhammad SAW. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja'faru Swadiq AS ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kwamba amesema: Mtu anayesoma Suratul Kauthar katika sala zake za faradhi na za suna, Mwenyezi Mungu amtamyweshwa maji ya hodhi ya Kauthar Siku ya Kiyama.   

Malaika wa Wahyi

Bibi Fatima al Zahra alizaliwa na kulelewa katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ambako Malaika wa wahyi na ufunuo walikuwa wakiingia na kutoka wakileta ujumbe wa Mola Mlezi. Alikulia katika nyumba ambayo ndiyo pekee sauti ya Allahu Akbar (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa) ilikuwa ikisikika katika zama za awali za Uislamu.

Baada ya kazi za kila siku, Bibi Fatima alikuwa akijipinda kwa ibada, dua na kumtaradhia Mola Karima.

Imam Ja'far Swadiq AS ananukuu kutoka kwa babu yake Imam Hassan bib Ali mwana wa Bibi Fatima AS akisema kwamba: "Mama alikuwa akisimama katika mihrabu ya ibada katika usiku za kuamkia Ijumaa hadi asubuhi. Alikuwa akiwaombea dua waumini wa kike na kiume bila ya kusema lolote kuhusu yeye mwenyewe. Siku moja nilimuuliza: "Mama! Kwa nini hauiombei nafsi yako kama unavyowaombea dua watu wengine? Alisema: "Mwanangu mpenzi! Jirani kwanza kisha nyumbani." Tasbihi na dhikri ambazo ni maarufu kwa jina la Tasbihatu Zahra alizofundishwa na baba yake kipenzi yaani Mtume Muhammad (saw) ni maarufu katika vitabu vya wanazuoni wa Shia na Suni.

Elimu ya Fatima Zahra SA

Tokea awali Bibi Fatima alijifunza elimu na maarifa katika nyumba na ufunuo na wahyi. Elimu na mambo yote ya siri aliyokuwa akifunzwa na baba yake yalikuwa yakiandikwa na mume wake Ali bin Abi Twalib AS.

Bibi huyu mtakatifu alifanya jitihada kubwa za kuwafunza wanawake wa Kiislamu maarifa ya dini hiyo. Alishika Qur'ani tukufu na kuanisika na kitabu hicho. Imepokelewa kwamba hata mtumishi wake, Bibi Fedha, ambaye pia alikuwa mwanafunzi mkubwa wa mtukufu huyo hakuwahi kuzungumza lolote au kujibu swali na mameno ya mtu yeyote bila ya kutumia aya za Qur'ani katika kipindi cha miaka 20. Alitumia aya za Qur'ani kueleza jambo au kuwasilisha muradi na makusudio yake.

Sala za salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika na Mitume wake zimshukie Bibi Fatima al Zahra.   

captcha