IQNA

Katibu Mkuu wa UN alaani mauaji ya mlinda amani CAR

19:40 - January 14, 2021
Habari ID: 3473556
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio liliofanya na wapiganaji wasiojulikana waliokuwa na silaha karibu na mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na kuua na kujeruhi akari wa vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo wakiwemo pia walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema shambulio hilo dhidi ya jeshi la ulinzi na vikosi vya usalama vya CAR na Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA karibu na Bangui limekatili Maisha ya mlinda amani mmoja kutoka Rwanda na mwinmgine kujeruhiwa.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za mlinda amani aliyepoteza maisha, watu na serikali ya Rwanda na amemtakia ahuweni ya haraka aliyejeruhiwa.

Uhalifu wa kivita

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imekumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walindamani wa Umoja wa Mataifa huenda ikawa ni uhalifu wa kivita.

Ametoa wito kwa mamlaka ya CAR kuchukua hatua zote za lazima ili kuhakikisha uwajibikaji kwa mashambulizi haya ya kikatili.

Pia amesema bado anatiwa hofu kubwa na kuendelea kuvurugwa kwa juhudi za kuleta utulivu kunakofanywa na makundi yenye silaha CAR na kutoa wito kwa pande zote kusitisha machafuko na kujihusisha katika majadiliano.

Amepongeza walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuendelea kujihusisha kwa karibu na wadau wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika juhudi za kulinda raia na kuleta utulivu wa kitaifa.

Katibu Mkuu amerejelea ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kufanyakazi kwa karibu na washirika wa kitaifa, kikanda na kimataifa kusaidia mchakato wa amani CAR.

Usalama waimarishwa

Wakati huo huo, kikosi cha MINUSCA kimetangaza kuimarisha hatua za usalama baada ya askari wake kutoka Rwanda kuuawa mjini Bangui Jumatano.

Magari ya kijeshi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MINUSCA yanaonekana kila mahali yakifanya doria katika mitaa ya mji mkuu wa CAR, Bangui.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Firmin Ngrebada amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao twitter: "Washambuliaji waliokuja kwa wingi kwa lengo la kuitwaa Bangui wamerejeshwa nyuma kwa nguvu kubwa." Ngrebada aidha amewataka raia wawe watulivu.

Mwanzo wa machafuko

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo,François Bozizé. Baada ya rais Mwislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

Djotidia alilazimishwa na nchi za kieneo kujiuzulu Januari mwaka 2014 na hapo mauaji ya Waislamu yakashika kasi zaidi. Kabla ya kuanza mgogoro, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa na wakaazi 130,000 Waislamu lakini sasa taarifa zinasema idadi hiyo ni chini ya 1,000.

Aidha watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao huku misikitr 436 kati ya misikiti yote 417 ya nchi hiyo ikiharibiwa au kubomolewa katika vita hivyo.

/3947696

captcha