IQNA

Hamas: Utawala wa Israel unatekeleza njama ya kuharibu sehemu za Msikiti wa Al Aqsa

20:15 - January 11, 2021
Habari ID: 3473547
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetahadharisha kuhusu mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kubomoa sehemu za Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem).

Katika taarifa, Hamas imelaani vikali njama hizo na kusema Msikiti wa Al Aqsa na uwanja wake wote ni milki ya Waislamu na hakuna yeyote mwenye haki ya kuvunja heshima ya eneo hilo takatifu.

Hamas imesema kuwa Wapalestina wako tayari kulinda eneo hilo takatifu hata kama itabidi watoe uhai wao mhanga katika kulinda qibla hicho cha kwanza cha Waislamu.

Aidha Hamase imetoa wito kwa Waarabu na Waislamu kote duniani kujitokeza katika kuutetea Msikiti wa Al Aqsa.

Jordan nayo pia imetoa taarifa na kulaani vitendo vya Israel kuuhujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa. Katika tukio la hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanza kuchimba eneo ambalo liko karibu na Ukuta wa Buraq ambao ni sehemu isiyotenganika na Msikiti wa Al Aqsa.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

3473671

captcha