IQNA

Waislamu Ethiopia wataka walioharibu msikiti mkongwe zaidi Afrika waadhibiwe

21:24 - January 08, 2021
Habari ID: 3473537
TEHRAN (IQNA) – Baraza Kuu la Kiislamu Ethiopia limetaka wale wote waliohusika katika kuuhujumu na kuuharibu Msikiti wa al-Najashi katika eneo la Tigray waadhibiwe.

Katika mkutano na waandishi habari Ijumaa hii, Sheikh Qassim Muhammad Tajuddin , Katibu Mkuu wa Baraza la Kiilamu Ethiopia amelaani vikali hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Najashi wakati wa vita vinavyoendelea katika jimbo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo na kutaka wahusika wote wa jinai hiyo wakamatwe na wafikishwe kizimbani.

Amesisitiza kuwa: “Tunaitaka serikali iwasake waliotekeleza jinai hiyo na pia hatua zichukuliwe za kuukarabati msikiti huo ambao nembo ya Uislamu na turathi ya kihistoria ya Ethiopia.”

Sheikh Tajuddin ameendelea kusema kuwa: “Baraza Kuu la Kiislamu linafuatilia kwa karibu kadhia ya kuharibiwa msikiti huo na tayari kamati maalumu imetumwa katika eneo la tukio kufanya uchunguzi na wananchi wa Ethiopia wa watafahamishwa matokeo ya uchunguzi huo.”

Msikiti wa kale zaidi barani Afrika wa al-Najashi waharibiwa kwa makombora huko Tigray

Msikiti wa al-Najashi upo katika mji wa Wukro katika eneo la Tigray, yapata kilomita 800  kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Eneo hilo limekuwa likishuhudia mapigano makali baina ya majeshi ya serikali na kundi la TPLF ambalo limekuwa likitekeleza mkakati wa kujitenga na Ethiopia.

Mwaka 2015 shirika moja la misaada la Uturuki lilizindua mradi wa kuukarabati Msikiti huo, na kuongeza kuwa lilitaka ''kuhifadi turathi'' hiyo ya kale na kufanya eneo hilo kuwa kivutio cha ''Utalii wa kidini''.

Shirika lisilo la kiserikali la Ubelgiji, linaloendesha shughuli zake Afrika, mnamo Desemba 18 liliripoti kwamba Msikiti wa al-Nejashi "ulilipuliwa kwa bomu kwanza na baadaye kuporwa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea".

" Vyanzo vya habari ndani ya Tigray vinasema kwamba watu kadhaa walifariki wakijaribu kulinda Msikiti huo.

Serikali ya Ethiopia tayari imeahidi kukarabati msikiti huo wa kale ulioharibiwa mwezi uliopita katika mzozo uliolikumba jimbo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo.

Msikiti wa al-Najashi uliripotiwa kushambuliwa kwa makombora, vitu ndani kuibwa na makaburi ya kihistoria ya viongozi wa Kiislamu kuharibiwa.

Wakazi wa eneo hilo wanaamini kuwa, Msikiti wa al-Najashi ulijengwa na Waislamu wa kwanza kuhamia Afrika enzi ya Mtume Muhammad SAW.

Waislamu katika eneo hilo wanaamini kwamba maswahaba 15 wa Mtume Muhammad SAW walizikwa katika makaburi hayo yaliyoharibiwa.

Pia wanasema Msikiti huo ni wa kale zaidi Afrika, japo wengine wanaamini msikiti wa kale zaidi unapatikana nchini Misri.

3946344

captcha