IQNA

Usajili wa Mashindano ya Qur'ani ya Dubai

10:20 - December 12, 2018
Habari ID: 3471768
TEHRAN (IQNA)- Usajili umeanza kwa wanaotaka kushiriki katika duru ya 20 ya mashindano ya kimataifa ya Dubai nchini UAE ambayo rasmi yanajulikana kama Mashindano ya Qur'ani ya Sheikha Hind Bint Makhtoum.

Wasimamizi wanasema siku ya mwisho ya kujisajili katika mashindano hayo ya Qur'ani ni Januari 17.

Kwa mujibu wa Ibrahim Mohammed Bu Melha, mshauri wa Mtawala wa Dubai katika Masuala ya Utamaduni ambaye pia ni mwenyekiti wa Zawadi ya Kimataifa ya Qur'ani ya Dubai (DIHQA), mashindano hayo ya kila mwaka yatakuwa na vitengo nane na washiriki ni raia wa UAE pamoja na raia wa kigeni wanaoishi nchini humo.

Amesema kitengo cha kwanza kitakuwa cha kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu na vitengo ya pili vitakuwa vya wenye kuhifadhi Juzuu 20 na 10. Kitengo cha nne cha mashindano kitakuwa kwa wale wenye kuhifadhi Juzuu tano huku kitengo cha tano kikiwa maalumu kwa raia wa kigeni wanaoishi UAE ambao wamehifadhi Juzuu tano na walio chini ya umri wa miaka 10.

Bw. Bu Melha ameendelea kusema kuwa: "Kitengo cha sita ni cha raia wa UAE waliohifadhi Juzuu tatu na walio na umri wa chini ya miaka 10: kitengo cha saba ni cha waliosilimu ambao wamehifadhi juzuu moja na kitengo cha nane ni cha watu wanaojitahidi kuhifadhi Qur'ani ambao wamehifadhi sehemu yoyote ya Qur'ani."

Aidha amesema raia wa kigeni wanaoshiriki wanapaswa kuwa na kibali rasmi au visa ya kuishi UAE.

3467445

captcha