IQNA

Mtoto wa miaka 7 Uingereza amehifadhi Qur'ani kikamilifu

10:47 - December 04, 2018
Habari ID: 3471761
TEHRAN (IQNA)- Mtoto wa miaka 7 kutoka mji wa Luton nchini Uingereza amehifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu ikiwa ni katika kufuata nyayo za dada yake ambaye pia alifanikiwa kufanya hiyo miaka miwili iliyopita wakati akiwa na umri huo huo.

Mtoto wa miaka 7 Uingereza amehifadhi Qur'ani kikamilifu"Nilihisi kana kwamba niko kwenye ndoto. Sikuwahi kudhani kuwa angepata mafanikio haya. Kwa hakika Allah SWT ametubariki kuweza kufanikiwa katika safari hii," amesema mama mzazi wa Yusuf Aslam.

"Allah SWT anasema atakurahisishia ukijitahidi na kwa kweli amejitahidi," aliongeza kusema.

Dada yake Yusuf, Maariya, alipata mafanikio kama hayo miaka miwili iliyopita na hivyo aliweza kumsaidia kaka yake kuhifadhi Qur'ani.

"Maariya alinisaidia wakati nilikuwa na shughuli nyingi. Maariya ana uwezo wa kipekee katikakuhifadhi Qur'ani na amekuwa akitoa msaada wake wakati alipotakiwa," mama yake amebainisha.

Aidha anasema safari ya kuwawezesha watoto hao wawili kuhifadhi Qur'ani haikuwa rahisi lakini hatimaye wamefanikiwa. "Nimeacha kazi yangu ili kujikita katika kuwalea watoto wangu na kuhakikisha kuwa wanapata malezi bora ya Kiislamu na wanafanikiwa katika masomo yao. Kama mzazi, nimebarikiwa kwa kuwa na watoto wawili ambao wanashirikiana nami na wanazingatia maadili bora na kutumia wakati wao ipasavyo, " amesema mama mzazi wa watoto hao wawili waliohifadhi Qur'ani.

Anatoa ushauri kuwa, wazazi wenyewe wanapaswa kujifunza Tajwidi ili kuwafunza watoto wao na anasisitiza kuwa hilo ni jambo la dharura.

/3467369

captcha