IQNA

Kituo Kipya cha Kiislamu kukabiliana na misimamo mikali Mombasa, Kenya

0:15 - March 14, 2018
Habari ID: 3471428
TEHRAN (IQNA)- Kituo kipya cha Kiislamu kimefunguliwa katika mjini Mombasa, Kenya katika mtaa wa Majengo kwa lengo la kukabiliana na misimamo mikali ya kidini.

Kituo hicho cha Kiislamu, kinachojumuisha Masjidul Zawiya al-Qadiriyya, kimefunguliwa mwishoni mwa wiki na Sheikh Abdulkadir al-Ahdal mwenyekiti wa Baraza la Sufi la Afrika Mashariki. Akihutubu katika kikao hicho cha ufunguzi, Sheikh Al-Ahdal alisisitiza umuhimu wa maeneo ya ibada kutumiwa katika kukabiliana na misimamo mikali ya kidini miongoni mwa vijana sambamba na kueneza ujumbe wa amani.

Sheikh Al Ahdal ametoa wito kwa maulamaa wa Kiislamu kukabiliana na ugaidi huku akisisitiza kuwa umefika wakati sasa kwa maulamaa kusimama na kuwapinga wale wanaoeneza hitilafu na kuvuruga umoja nchini Kenya. Amesema wahubiri Waislamu wanapaswa kukaa na vijana na kuwazuia kutumbukia katika mtego wa misimamo mikali na ugaidi sambamba na kuwafunza kuhusu amani, umoja na kuishi pamoja kwa maelewano. Sheikh Al Ahdal amebaini kuwa, Msikiti wa Zawiya al-Qadiriyya unalenga kueneza ujumbe wa amani, umoja na maisha ya maelewano miongoni mwa watu wa dini mbali mbali na kwamba msikiti huo pia utajumuisha jitihada za kukabiliana na misimamo mikali katika jamii.

“Tunajua Uislamu umetekwa na watu wachahce wenye misimamo mikali na tuna azma ya kukabiliana na fikra hizo,” ameongeza.

Mwanazuoni huyo maarufu wa Kiislamu Afrika Mashariki amesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya amani na huo ni msingi ambao utahimizwa sana katika msikiti uliofunguliwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa kituo hicho cha Kiislamu, Sheikh Abdullah Mohammad wa Malindi amesema kuna wengi wasioufahamu Uislamu na kwa msingi huo kuna haja ya kuhubiri  misingi ya amani na kustahamiliana miongoni mwa vijana. Aidha amesisitiza kuwa Uislamu unapinga kuuawa watu wasio na hatia. Halikadhalika amesema Uislamu unahimiza umoja,maelewano na udugu na kwamba kuna haja ya kufuata mafundisho hayo ili ufanisi upatikane.

3699186

captcha